Na Hassan Abbas, Addis Ababa
Mpango
wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) umempata Mwenyekiti wake
mpya na mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo mkubwa kufuatia
kuchaguliwa kwa Rais wa Liberia, Mama Ellen Johnson Sirleaf.
Rais
Sirleaf alichaguliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika
Wachama wa APRM uliofanyika Jumapili jioni mjini hapa.
Katika
uchaguzi huo ambapo Rais Jakaya Kikwete aliwakilishwa na Naibu Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim, Mama
Sirleaf licha ya kuweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza pia anakuwa
Mwenyekiti wa tatu wa Marais wa APRM tangu Mpango huo ulipoanzishwa
mwaka 2003.
Sirleaf
alichaguliwa kwa kauli moja kufuatia mpinzani wake Rais wa Senegal,
Marcky Sall kujitoa. Rais Sall tayari ni Mwenyekiti wa taasisi nyingine
ya AU, NEPAD.
Katika
mkutano huo, Wakuu hao wa Nchi za APRM pia walitumia mkutano huo
kumteua kiongozi wa Jopo la Tathmini ya Tanzania, Wakili Akere Muna
kutoka Cameroun kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri kwa Marais wa APRM
na aliyekuwa Balozi wa Rwanda nchini, Fatma Ndangiza kuwa Makamu wake.
Akizungumza
mara baada ya uchaguzi huo, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema
Twalib aliwapongeza viongozi hao wapya katika utendaji wa APRM Afrika
akiuita uongozi huo kuwa ni “timu ya ushindi.”
APRM
ni Mpango ulioanzishwa na Serikali za Umoja wa Afrika kwa lengo la
kuhusisha wananchi wao katika kila nchi ili kufanya tathmini za mara kwa
mara za utawala bora ili kubaini changamoto za kufanyiwakazi na mambo
mazuri ya kuendelezwa.
Mpango
huo ulianzishwa rasmi miaka 10 iliyopita na Tanzania ilijiunga Mei 26,
2004 na Bunge likaidhinisha Mchakato huo kuanza hapa nchini. Tayari APRM
Tanzania imekwishakamilisha ripoti ya kwanza ya Hali ya Utawala Bora
Tanzania na Serikali itaanza kufanyiakazi changamoto hizo katika bajeti
za kila mwaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni