MWANAMUZIKI mkongwe aliyestaafu muziki akiwa na bendi ya Msondo Ngoma, Muhidini Maalim Gurumo, ameandaliwa shoo mbili za kumuaga, moja wapo ikipangwa kufanyika Oktoba 11, ikiwa ni VIP, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Shoo nyingine kwa wapenzi wote itafanyika Novemba Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa TCC Sigara Chang’ombe, jijini Dar es Salaam, zote zikiwa na lengo la kumuaga kwa heshima mwanamuziki huyo na kumpa nafasi ya kuyamudu maisha yake baada ya kuachana na muziki.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa shoo hiyo iliyopewa jina la (Gurumo 53), Asha Baraka, alisema kuwa ni heshima kuwa na mwanamuziki kama Gurumo, hivyo wadau wameamua kuandaa shoo hizo za kumtafutia fedha mkali huyo.
Alisema wazo hilo limefanyiwa kazi kwa pamoja, akiwa na wadau kadhaa, akiwamo Said Mdoe Katibu wa Kamati hiyo, Richard Sakala mjumbe, Cosmas Chidumule, Waziri Ally, Said Kibiriti na Juma Mbizo, ambaye ndio mratibu wa Kamati hiyo.
”Lengo si kumpa karatasi za kuthamini mchango wake katika tasnia ya muziki wa dansi Tanzania, ila kuhakikisha kuwa anapata mwangaza wa maisha yake baada ya kuachana na muziki.
”Huyu ni mwanamuziki mwenye uwezo wa juu wakati huo, hivyo kwa sasa lazima sisi wadau tuhakikishe anajiweka katika ramani nzuri, ikiwa ni kutambua ataishi vipi nje ya muziki,” alisema. Naye Gurumo aliwaambia waandishi wa habari kuwa ameamua kuachana na muziki kwa sababu umri na afya yake hairuhusu kufanya kazi hiyo, hivyo asitokee mtu wa kupotosha ukweli wake huo.
”Nasikia watu wanasema naachana na muziki Msondo nikiwa na lengo la kurudi tena Sikinde, jambo ambalo si kweli kwa kuwa sioni nitamuimbia nani wakati nimechoka.
”Naomba kwa sasa kuwapa nafasi watu waliojitolea kunisaidia hasa kwa kuunda kamati hii ambayo nitapanda jukwaani kuimba mara ya mwisho, ukizingatia kuwa kazi yangu inahitaji kuagana na mashabiki wangu jukwaani na si mahali pengine,” alisema.
Katika hatua nyingine, mwanamuziki Cosmas Chidumule, alisema kuwa licha ya kuwa ameokoka, ila atapanda jukwaani kuimba na mzee Gurumo kama sehemu ya kutambua mchango wake. ”Nimeokoka lakini si sababu ya kunifanya nishindwe kumheshimu mwanamuziki ambaye nina uhakika mchango wake ulinifanya niwe juu katika muziki wa dansi Tanzania,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamati hiyo ambayo Mdoe ndio Katibu wake, taratibu zote zinaendelea ikiwa ni kuandaa nyimbo alizowahi kuimba na kuziweka katika mfumo wa kibiashara, ikiwamo mpango wa kuuza nyimbo zake katika makampuni ya simu za mikononi.
Mwenyekiti wa kamati ya kumuenzi Muhidin Maalim Gurumo, Asha Baraka, akizungumza jambo katika kutambulisha onyesho maalum la Gurumo litakalofanyika Oktoba 11 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam. Anayefuata upande wa kushoto wa Asha ni mzee Muhdini Gurumo, Juma Mbizo, na Said Kibiriti.
Asha Baraka na wanakamati katika kutambulisha onyesho maalum la Gurumo litakalofanyika Oktoba 11 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam. Anayefuata upande wa kushoto wa Asha ni mzee Muhdini Gurumo, Juma Mbizo, Cosmas Chidumule na Said Kibiriti. Kulia ni Katibu wa kamati Saidi Mdoe
Juma Mbizo, mratibu wa shoo hiyo, akionyesha mfano wa cd itakayouzwa ikiwa ni juhudi za kumuwekea mazingira mazuri mwanamuziki Muhdini Gurumo, baada ya kutangaza kustaafu muziki. Picha zote na Kambi Mbwana
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni