ONYESHO
kubwa ambalo ni uzinduzi wa Shindano la QS Queens 'Utamu Extra'
linalotarajiwa kufanyika Jumamosi ya kesho ya Juni Mosi katika Ukumbi wa
Dar Live, Mbagala, pia limepangwa kuwa sehemu maalum ya kuenzi mchango
wa msanii Albert Mangwea, aliyefariki nchini Afrika Kusini.
Ngwea
amepangwa kuletwa kesho Jumamosi kwa ajili ya maziko yake yaliyopangwa
kufanyika mkoani Morogoro, huku onyesho hilo la maombolezo likihudhuliwa
na wakali kibao wa muziki hapa nchini lilioandaliwa kwa muda mrefu na
kilele chake kuwa Jumamosi hii.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, leo
mchana, Meneja Masoko wa Kampuni ya QS Mhonda J Entertainment, Freddy
Felix, alisema kuwa shindano hilo litafanyika pia katika mikoa
mbalimbali kwa ajili ya kupata warembo 20 watakaoishi katika Jumba moja
kwa ajili ya kupata kimwana huyo wa QS Queens.
Alisema
kuwa wasanii wengi wamepangwa kupanda jukwaani kwa ajili ya kuomboleza
msiba huo, akiwamo Ney wa Mitego, Wanaume Halisi, ikiongozwa na Juma
Nature, MB Dog, Diamond, Inspector Haroun, Madee, H-Baba, Snura, Khadija
Kopa, Solid Ground Family na wengineo, wakiwamo wasanii chipukizi, Amor
na Shalviny.
“Wasichana
wote wanaotaka kushiriki shindano hili ambao ni kama uzinduzi wake,
watajiandikisha katika fomu maalum ukumbini hapo, ambapo baadaye
watatafutwa wengine ambao wote wataishi kwa miezi miwili katika nyumba
moja itakayotembelewa na watu mbalimbali.
“Huku
mshindi akijishindia gari la kifahari, pia wanapokuwa katika jumba hilo
kila siku mtu atalipwa kadri tutakavyokubaliana, huku tukiamini kuwa
huu utakuwa ni mwanzo mzuri katika shindano hili,” alisema Felix.
Kwa
mujibu wa Felix, shindano hili kabla ya kupatikana warembo hao
litatembelea mikoa kadhaa ya Tanzania Bara, kama vile Mwanza, Tanga,
Morogoro, Mbeya, Iringa na kwingineko kwa ajili ya kutafuta msichana
mmoja wa kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Aidha
QS ilitangaza kuwa mabinti wanaotakiwa kushiriki katika shindano hilo ni
wale wenye vipaji maalum na uwezo wowote wa kupambanua mambo, huku
kigezo cha elimu kikiwekwa pembeni.
Shindano
hilo pia litaonyeshwa katika vituo vya Channel Ten, DTV, Clouds, ambapo
huko kote wadau na wapenzi wa mambo ya urembo na burudani watapata
fursa ya kuwapigia kura washiriki kabla ya siku ya kilele chake
kitakachofanyika baadaye mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni