Na Mwandishi Wetu
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imetoa mwongozo unaoruhusu kuanza rasmi kwa
uundwaji wa Mabaraza ya Katiba ya asasi, taasisi na makundi mbalimbali
kwa lengo la kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya katiba
inayotarajiwa kutolewa na Tume hiyo hivi karibuni.
Kwa
mujibu wa mwongozo ulitolewa na Tume hiyo leo (Jumatano, 29 Mei, 2013)
na kusainiwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba, mwongozo
utatumika kwa miezi mitatu kuanzia keshokutwa, Juni 1 hadi Agosti 31
mwaka huu.
“Mabaraza
haya ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye malengo
yanayofanana yatajadili na kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba,” amesema
Jaji Warioba na kuongeza kuwa maoni hayo yanaweza kuwasilishwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kwa njia ya randama, barua, andiko, muhtasari wa
makubaliano.
Mwongozo
huo, ambao utachapishwa katika magazeti mbalimbali ya siku ya Alhamisi
(Mei 30, 2013) na kurudiwa tena Jumatatu (Juni 3, 2013), pia unapatikana
katika tovuti mbalimbali ikiwemo ya Tume hiyo (www.katiba.go.tz) na ukurasa wa facebook wa Tume hiyo (Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania).
Kwa
mujibu wa maelezo ya Jaji Warioba katika mwongozo huo, mabaraza hayo ya
taasisi yanaundwa kwa mujibu wa kifungu cha 18 (6) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 kinachoitaka Tume kuruhusu Asasi,
Taasisi na Makundi ya Watu wenye malengo yanayofanana kuandaa mikutano
kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wao kutoa maoni yao juu ya Rasimu
ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume.
Katika
mwongozo huo, Jaji Warioba ametaja taasisi zinazoweza kuunda Mabaraza
hayo kuwa ni pamoja na Jumuiya ya Kidini, Chama cha Siasa, Asasi ya
Kiraia, Taasisi ya Elimu ya Juu, Chama cha Wafanyakazi, Chama cha
Wakulima, Chama cha Wafugaji, Chama cha Wanahabari na Baraza la Watoto.
Taasisi
nyingine zinazoweza kuunda mabaraza hayo ni taasisi ya Wafanyabiashara,
Mabaraza ya Wanawake, Taasisi ya Kitaaluma, Baraza la Vijana, Baraza la
Wazee, Jumuiya ya Kijamii (CBO) na Chama cha Waajiri. Nyingine ni Chama
cha Wanasheria, Umoja wa Watanzania waishio Nchi za Nje, Wizara, Idara
na Taasisi za Serikali, na Kundi au makundi ya watu wenye malengo
yanayofanana au wale wenye mahitaji maalum katika jamii.
Kuhusu
gharama za uendeshaji, mwongozo huo unaelekeza kuwa Mabaraza ya Katiba
ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye Malengo Yanayofanana,
yatagharimia taratibu zote za uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba hayo.
Kwa
mujibu wa Jaji Warioba katika mwongozo huo, ili kuiwezesha kuratibu kwa
ufanisi mchakato wa kukusanya maoni kuhusu Rasimu ya Katiba, kila Asasi,
Taasisi na Makundi ya Watu wenye malengo yanayofanana yatakayounda
Mabaraza ya Katiba itatoa taarifa ya maandishi ya kusudio la kuunda,
kuendesha na kusimamia Mabaraza ya Katiba.
Taarifa
hiyo itawasilishwa katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba moja
kwa moja – Makao Makuu, Mtaa wa Ohio - Dar es salaam au Ofisi Ndogo Mtaa
wa Kikwajuni Gofu Jengo la Mfuko wa Barabara Zanzibar. Taarifa pia
inaweza kutolewa kwa Tume kupitia S.L.P. 1681, Dar es Salaam au S.L.P.
2775, Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni